Katika Mkakati wa kisiasa uliosukwa na chama tawala (CCM) kudhoofisha vyama vya upinzani Tanzania kwa ‘kununua’ wabunge, nusura hamahama hiyo imkumbe pia Mbunge wa Ubungo (CHADEMA), Saed Kubenea.
Chanzo chetu cha uhakika kinabainisha kuwa Kubenea ambaye alikuwa na mpango wa kukihama chama chake, kila kitu kilikamilika kwa kiwango kikubwa lakini alilazimika kubadili msimamo wake baada ya kifo cha mfanyabiashara tajiri, Reginald Mengi ambaye alikuwa Mhimili katika kufanikisha zoezi hilo.
Mengi alihusikaje?
Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa katika mchakato huo, marehemu Mengi ambaye alikuwa “mzee wa karibu” na Kubenea, alipewa jukumu la kuhakikisha mbunge huyo anahama CHADEMA na kujiuga na CCM ili kuongeza idadi ya wabunge waliokuwa wamekihama chama hicho kikuu cha upinzani.
Katika mazungumzo kati ya Kubenea na Mengi yaliyofanyika nyumbani kwa marehemu, kwa nyakati tofauti, mbunge huyo aliridhia kupoea kiasi cha Shilingi milioni 70.
Hata hivyo, katika kufunga mkataba huo (wa maneno), Kubenea alipokea Shilingi milioni 50, huku kiasi kilichobaki wakikubaliana kukipokea siku akitangaza mbele ya waandishi wa habari, kukihama chama chake. Ilipangwa apokewe na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole siku ya Alhamisi ya Machi 21, 2019 ndani ya jengo la Ofisi Ndogo ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam.
Nini kilikwamisha mpango huo?
Mpango huo haukufanikiwa kwa kuwa Kubenea hadi Machi 20, 2019 aliamua “kukimbiakimbia” akitaka malipo kukamilika kabla ya kurejesha kadi ya CHADEMA na kutangaza kuunga mkono juhudi.
Hadi mauti yanamkuta mzee Mengi, Mei Mosi, 2019 akiwa Dubai, Falme za Kiarabu (UEA) na hadi kuvunjwa kwa Bunge la 11, Kubenea hakuwa amerudisha fedha alizopewa huku akisisitiza kwamba hatahama CHADEMA na kwamba anatarajia kuteuliwa kuwania tena ubunge wa Ubungo.
Kubenea amekuwa akikana kupokea kiasi chochote cha fedha kwa lengo la kuhama CHADEMA, huku akidai kwamba kuwepo kwa taarifa hizo ni mbinu za wale aliowaita wabaya wake kumchonganisha na chama chake.
Wakati wa msiba wa mzee Mengi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisikika akisema; “Kubenea tunakudai wewe na mzee ameondoka hujatekeleza.” Haikufahamika mara moja alikuwa akimaanisha nini.
Hamahama ilivyosukwa
Taarifa zinaeleza kuwa kila mbunge wa CHADEMA aliyehamia CCM ilipangwa apewe Sh. Milioni 70 kupitia kwa watu 10 ambao kimkakati CCM iliwategemea kufanikisha zoezi.
Miongoni mwa waliopewa kazi hiyo ni marehemu Reginald Mengi, Subash Patel, Mo Dewji, Mwita Christopher Gachuma na wengine. Katika kazi hiyo, wamo waliofanikisha wabunge wawili, watatu na wengine “kuambulia patupu.”
Wapo baadhi ya wabunge waliohamia CCM kutoka Chadema, walienda kwa mkopo na hadi sasa ama wamepewa Sh. mil 20 au 30 kwa ahadi ya kumaliziwa baadaye. Hata hivyo, kwa bunge kuvunjwa, huenda ndio “wameingizwa mjini.”
Leave a Reply