RCO wa mkoa Kilimanjaro, Bwana Dotto Mdoe ameingia katika kashfa baada ya kuachia gari lililokuwa likishikilia Kituo kikuu cha Polisi kama kielelezo hata kabla mtaalamu aliyetumwa kutoka ofisi ya DCI hajatoa ripoti yake ya ukaguzi.
Gari hilo aina ya Toyota Hilux namba T525 DHX ni mali ya mmiliki wa mabasi ya Capricorn, Bwana George Mberesero na liliibwa kwa kula njama kati ya mmiliki wa gereji moja inayoitwa WAG, Bwana Godfrey Mtui na mtu anayejifanya Afisa Usalama wa Taifa (TISS) Bwana Emmanuel Kimbe.
Taarifa za ndani kabisa na za kuaminika, zinadai gari hilo lilipokamatwa na kupelekwa kituoni na kukaguliwa lilikutwa limefutwa namba za chasis na kugongwa namba nyingine ambazo ni LN107-0008870 na kubandikwa namba T807 ADR ambazo ni gari la mwaka 1987 wakati gari ni la mwaka 2000.
Kadi ya gari iliyofaulishwa yaani T 807 ADR inaonyesha gari lenye kadi hiyo linatumia Diesel wakati gari la Bwana George Mberesero linatumia Petroli.
Mtoa habari wetu anasema pamoja na ushahidi wote huo, Tarehe 02 Julai 2020 RCO alitoa amri kielelezo hicho alirudishiwe Dkt. Joseph Msaki aliyeuziwa gari hilo, hata kabla ya ripoti ya mtaalamu wa magari kutoka ofisi ya DCI kurudisha ripoti yake.
Aibu kubwa imempata RCO huyo kwani ripoti ya mtaalamu wa magari kutoka ofisi ya DCI iliyorudishwa Moshi tarehe 04 Julai 2020 imethibitisha namba za chasis za gari la Bwana George ambalo RCO alimkabidhi mtuhumiwa zilichezewa na kugongwa nyingine lakini tayari RCO alishamrudishia aliyekutwa nalo.
Watu wanaona hiki alichokifanya RCO ni kinyume na mwenendo wa Jeshi la Polisi na dharau kwa DCI ambaye alituma mtaalamu kutoka Dar hadi Moshi ambaye ripoti yake imemuumbua RCO.
Leave a Reply