Mkakati wa timu ya Makonda kuhakikisha zinapatikana kura nyingi za maoni kutoka kwa wajumbe wa mkutano mkuu Jimbo la Kigamboni uligubikwa kwa rushwa, imebainika.
Rushwa hiyo iliyotembezwa waziwazi kwa wajumbe wa mkutano huo uliomalizika leo, imedhihiri baada ya wapambe wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuanza kuwatukana na kuwatisha baadhi ya wajumbe hao.
Waliokula pesa na kuhisiwa kutompigia kura waitwa wahuni
Mara baada ya matokeo ya wagombea hao wa CCM kutangazwa, wapambe wa Makonda, wengi wakiwa nje ya ukumbi wa mkutano walisikika wakitukana na kuwaita wajumbe waliodai wamekula pesa zao kuwa ni “wahuni.”
Mmoja wa wapambe hao, Jack Pemba aliyeonekana mara kwa mara maeneo ya Kigamboni tangu wiki iliyopita akiwa na Makonda, alisema “Kigamboni watu wajinga sana, wanaacha mpiganaji?” hapa akionekana kumaanisha Makonda.
Jack Pemba anatajwa katika safari zake za Kigamboni kuwa alikuwa akifuatana na timu ya wapambe wenzake kusaka wajumbe na kuwapa rushwa.
Katika uchaguzi huo, Makonda aliambulia kura 122 huku mbunge aliyemaliza muda wake, Dkt. Faustine Ndugulile akiibuka kidedea kwa kura 190.
Jack Pemba ambaye amekuwa akijinadi kuwa “rafiki na ndugu tajiri” wa Makonda, aliwasili nchini Jumanne ya wiki iliyopita.
Pemba aliwaeleza marafiki zake kwamba amekuja “kumaliza kazi Kigamboni” kwani ana mzigo wa kutosha (pesa).
Pamoja na Kigamboni maeneo mengi kulikofanyika uchaguzi huo yamedaiwa kugubikwa na vitendo vya rushwa, huku wabunge waliomaliza muda wao wakitajwa kutumia fedha nyingi kuwahonga wajumbe.
Mmoja wa wagombea kutoka Lindi amesikika akilalamika kuwa mafao ya wabunge waliomaliza muda wao yametumika kuminya haki katika mchakato huo.
1 Comment