Timu ya kampeni ya mgombea Ubunge katika Jimbo la Kawe kupitia CCM, Askofu Josephat Gwajima imeanza kampeni za nyumba kwa nyumba, ikiomba samahani kwa niaba ya mgombea.
Taarifa zilizotufikia zinaeleza kuwa timu hiyo ya kampeni, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), juzi ilikuwa Kata ya Bunju, ikiongozwa na wenyeviti na wajumbe wa Serikali za Mitaa.
Katika kampeni hizo, timu hiyo imekuwa ikiomba msamaha kwa “lolote baya alilofanya ama kusema” mgombea wao, Askofu Gwajima.
Inaelezwa kwamba pamoja na baadhi ya wakazi kuhoji makosa ya Askofu Gwajima, timu hiyo imekuwa ikisema kwamba “kila binadamu ana makosa, sasa huenda alikosea na kukwaza baadhi ya watu mahali fulani, hivyo hakuna ubaya kuomba msamaha.”
Timu hiyo imekuwa ikiingia nyumba hadi nyumba na kuanza kuuliza endapo kuna wanafamilia ambao wana kadi za kupigia kura na baada ya hapo, huendelea na kampeni kwa Gwajima, huku suala la msamaha likisisitizwa zaidi.
Askofu Gwajima amekuwa akituhumiwa kuwakwaza Waislamu na Wakatoliki kwa baadhi ya kauli zake wakati wa mahubiri yake kanisani kwake, Ufufuo na Uzima.
Leave a Reply