Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi ameweka kambi Zanzibar ili kuongeza nguvu katika kampeni za ushindi kwa mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Taarifa zilizotufikia zinaeleza kuwa Mzee Mwinyi, ambaye ni baba mzazi wa mgombea urais Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, amepewa makazi jirani na eneo la kupanga mikakati ya ushindi kwa mgombea huyo, Fumba.
Timu binafsi ya mikakati ya ushindi imeweka makazi yake Fumba. Hii inaundwa na ndugu, marafiki wa karibu wa Dk. Mwinyi. Timu nyingine inayoratibiwa na CCM iko Kisiwandui ikijumuisha makada na wapanga mikakati kutoka taasisi nyingine nyeti.
Dk. Mwinyi anachuana vikali na mgombea wa ACT- Wazalendo, Maalim Seif Shariff Hamad. Kila mmoja anapewa nafasi ya kushinda urais katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba 28, 2020.
Wachambuzi wa siasa na uchaguzi wa Zanzibar wanampa Maalim Seif nafasi kubwa ya ushindi, endapo kutakuwa na haki na uhuru wa kutangaza mshindi halali.
Leave a Reply