Zanzibar kumekucha: Dkt. Mwinyi asaka muafaka na Maalim Seif

Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amemuomba Mufti wa Zanzibar, Salehe Kaab, kukutana na Maalim Seif Shariff Hamad ili kumfikishia ‘ujumbe wake’.

Taarifa zilizotufikia jioni ya leo zinaeleza kuwa Mufti Kaab tayari ameomba miadi ya kukutana na Maalim Seif sikiu ya Jumapili, Novemba 8, 2020

Chanzo cha IMEVUJA kimeeleza kwamba Mufti Kaab amebeba ujumbe wa Rais Dkt. Mwinyi unaoomba Maalim Seif kuridhia wito wake ili kujadili mustakabali wa amani ya visiwa hivyo na watu wake.

Habari kutoka Ikulu ya Zanzibar zinaeleza zaidi kuwa Dkt. Mwinyi hapendezwi na siasa za mgawanyiko visiwani humo hivyo ameamua kuwepo maridhiano ya pamoja baina ya Serikali, Chama tawala (CCM) na wapinzani.

Maalim Seif ni Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo ambaye pia alikuwa mgombea Urais wa visiwa hivyo akichuana vikali na Dkt. Mwinyi. Mshindi alitangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuwa ni Dkt. Mwinyi.

Wakati wa zoezi la kupiga kura ya awali, Oktoba 27 na siku ya umma kufanya zoezi hilo (Oktoba 28), kuliibuka vurugu maeneo kadhaa ya Pemba na Unguja na kuripotiwa Vikosi vya Usalama kutumia nguvu ya ziada kutuliza, huku ikielezwa kuwepo kwa baadhi ya watu kuuawa na wengine kujeruhiwa.