Matokeo ya Uchunguzi wa Kushambuliwa kwa Tundu Lissu kutolewa hadharani

Ofisi ya mawakili wa kimataifa, Amsterdam and Partners inayoshika mikoba ya kumwakilisha Tundu Lissu kisheria, imesema inajiandaa kutangaza matokeo ya uchunguzi juu ya kushambuliwa kwa mteja wake.

Taarifa zinaeleza kuwa mawakili hao wanajiandaa kutangaza matokeo ya uchunguzi wao muda wowote kuanzia sasa baada ya kile kinachoelezwa “Serikali kushindwa majukumu yake.”

Inaelezwa kuwa mawakili hao mara baada ya kupewa kandarasi ya kumsimamia masuala yote ya sheria kwa mteja wao Septemba 2018, moja ya kazi zake ilikuwa kupata ukweli kuhusu kushambuliwa kwa Lissu.

Kampuni hiyo kubwa ya mawakili ina kitengo cha maofisa wabobezi wa uchunguzi wa mashambulizi kwa watu maarufu duniani.

Lissu, akiwa Mbunge wa Singida Mashariki kupitia CHADEMA, alishambuliwa Septemba 7, 2017 akiwa Dodoma na wanaoelezwa na serikali kuwa watu wasiojulikana.

Tunazo taarifa kuwa kampuni ya mawakili hao wa Lissu, Amsterdam and Partners yenye ofisi zake Washington DC, Marekani na London, Uingereza, ilifanya uchunguzi wake kwa kutumia maelezo ya Lissu, dereva wake, mwenyekiti wa CHADEMA,  Freeman Mbowe na watu wengine.

Kwamba uamuzi wa kutangaza matokeo hayo ya uchunguzi wa shambulio dhidi ya Lissu unafuatia kimya cha serikali katika suala hilo.

Tayari kampuni hiyo iliiandikia barua Serikali ya Tanzania ikiitaka kufanya uchunguzi na kutoa matokeo juu ya kushambuliwa kwa mteja wake.

Sehemu ya barua hiyo ya Julai 22, mwaka jana, iliyotumwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani, inasema – “Serikali ya Tanzania imekwepa jukumu lake hili kwa muda mrefu, sasa ni muafaka kutimiza wajibu wake kwa raia wake, Tundu Lissu.”

Serikali ya Tanzania hadi sasa haijawahi kujibu barua hiyo.

Lissu anatarajia kurejea nchini Julai 27, akitua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam – Jumatatu saa 7.20 mchana.