Mrisho Gambo alitembeza Rushwa, kama Makonda

YAMEIBUKA madai mazito ya uwepo wa matukio ya rushwa kwenye kinyang’anyiro cha kumsaka mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), atakayepeperusha bendera ya chama hicho kwenye nafasi ya ubunge jimbo la Arusha Mjini. Mbinu alizotumia Makonda huko Kigamboni zinafanana.

Aidha msimamizi wa Uchaguzi huo adaiwa kuonyesha upendeleo wa wazi kwa baadhi ya wagombea kwa kuzuia mmoja wa wagombea asiulizwe maswali licha ya wajumbe kunyoosha mikono na wengine kuamua kusimama kabisa lakini hakuruhusu

Madai hayo yameibuliwa kwa nyakati tofauti muda mfupi baada ya matokeo ya Uchaguzi huo kutangazwa ambapo, Mrisho Gambo aliibuka mshindi kwa kupata kura 333, akifuatiwa na Philemon Mollel aliyepata kura 68 huku Albert Msando akipata kura 19.

Uchaguzi huo uliwakutanisha wagombea 90 ambapo wengi hawakupata kura hata moja huku wachache wakipata kura moja na wengine mbili.

WALIOHONGWA HAWAKUMALIZIWA KIASI CHA MWISHO

Kama ilivyokuwa kwa Kigamboni, madai ya uwepo uwepo wa matukio ya rushwa yaliibuka muda mfupi baada ya mkutano huo kumalizika kwani kulionekana baadhi ya wajumbe wakidai kuwa waliahidiwa kumaliziwa kiasi fulani cha fedha uchaguzi ukimalizika lakini ilishindikana kupatiwa kwani wachache ndiyo waliweza kupiga picha huku wengine wakishindwa kutokana na katazo lililotolewa ukumbini hapozwa.

Wapiga kura hao ambao hawakuwa tayari majina yao kuandikwa kwa kile walichodai kuwa wanajua sheria inakataza kutoa au kupokea rushwa hivyo wakijulikana wanaweza kuingia matatizoni.

Hata hivyo wengine walidai kuwa kuna viongozi wenzao wamepewa pikipiki lakini hawakukabidhiwa kadi ambayo walitakiwa waonyeshe picha ya kura waliyopiga ili wapatiwe ambapo nao kuna baadhi wanaweza kukwama kupatiwa kadi hizo kwani walishindwa kupiga picha japo kura walimpigia mgombea huyo.

MSIMAMIZI WA UCHAGUZI ANENA

Msimamizi wa uchaguzi huo, Mary Kisaka alisema kuwa yeye hakuona hao wajumbe wanaodaiwa kunyoosha vidole kutaka kumuuliza maswali Gambo.

“Kweli kabisa sikuona kama kuna mtu alinyoosha mkono kutaka kumuuliza maswali Gambo ningewaruhusu. Sikuwa na sababu ya kuzuia,” alisema Kisaka ambaye pia ni mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Arusha Mjini.

Aidha alisema wakati akiwa meza kuu akisimamia uchaguzi huo alidai kuwa baadhi ya wajumbe walikuwa wakimtumia ujumbe wa simu wakimtaka asiruhusu maswali kwani angesababisha kura kuhesabiwa gizani, jambo lililomlazimu kupeleka uchaguzi mbio.

Aliongeza kuwa hakuwa na sababu ya kumbeba Gambo kwani licha ya kuwa msimamizi wa uchaguzi lakini ni mpiga kura halali wa kikao hicho lakini Gambo hakuwahi kumuomba kura zaidi ya kukutana ukumbini.

“Hata wakati nimefika nilikuta wajumbe wametawanyika pale nje ya ukumbi nilipita karibu na Gambo nikamsemesha lakini hakuonekana kunitilia maanani kwani alinipisha akaelekea upande tu sikuwa na sababu ya kumbeba,” alisisitiza Kisaka.

Hata hivyo alieleza kuna wakati alikataa maswali waliyoulizwa wagombea yasijibiwe huku akitolea mfano swali aliloulizwa mgombea, Philemon Mollel maarufu kama Monaban ambalo alidai halikuwa sahihi kuelekezwa kwa mgombea huyo.

KATIBU WA CCM ANENA

Katibu wa CCM wilayani hapa, Denis Mwita alisema ofisi yake haijapokea malalamiko yoyote tokea kwa wagombea hao ingawa alisema kuwa milango iko wazi kwani wanatakiwa kuwasilisha malalamiko yao ndani ya saa 24 tokea matokeo yatangazwe.

“Pale ukumbini wagombea wote walisaini fomu ya kukubali matokeo. Nilitangaza pale yeyote mwenye malalamiko ayawasilishe kwa maandishi na ushahidi na mpaka sasa sijapokea malalamoko yoyote,” alisema Mwita.

Hata hivyo alisema kuwa hayo madai ya wapiga kura kutakiwa kupiga picha karatasi za kura kuonyesha wamempigia nani walizipata ndiyo sababu walipiga marufuku hakuna kupiga picha fomu hiyo.

“Kuna picha yoyote mmeona mtu aliyepiga picha? Kwa sababu hizo tetesi sisi tulizisikia kuwa kuna watu wameambiwa wapige picha kura wamempigia nani waende wakaonyeshe. Ndiyo sababu nilimwambia msimamizi wa uchaguzi atangaze pale hakuna mtu kupiga picha,” alisisitiza Mwita.